Jumanne 27 Oktoba 2026 - 09:59
Mapambano ya Imam Khomeini (r.a.) dhidi ya sheria ya kinga ya kisheria kwa Wamarekaniilikuwa chavhu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hawza/ Ayatullah Qurbanali Dori Najafabadi, katika darsa yake ya bahthi kharij ya jana, huku akigusia mapambano ya kihistoria ya Imam Khomeini (r.a.) dhidi ya sheria ya kapitulasyon (kinga ya kisheria kwa raia wa Marekani), aliitaja hatua hiyo kuwa miongoni mwa vipindi muhimu vya mapambano dhidi ya utawala wa Pahlavi. Aidha, alisisitiza nafasi ya wanazuoni katika kuielimisha jamii na kuweka mazingira ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Arak, Ayatullah Qurbanali Dori Najafabadi, katika darsa yake ya bahthi kharij ya jana, huku akigusia mapambano ya kihistoria ya Imam Khomeini (r.a.) dhidi ya sheria ya kapitulasyon, alitaja hatua hiyo kuwa miongoni mwa vipindi muhimu vya mapambano dhidi ya utawala wa Pahlavi. Alisisitiza pia nafasi ya wanazuoni katika kuielimisha jamii na kuweka mazingira ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Akizungumzia misimamo thabiti ya Imam Khomeini (r.a.) dhidi ya sheria ya kapitulasyon, alisema: “Imam Khomeini, kwa kuingia katika uwanja wa mapambano, aliwahamasisha wanazuoni kujipanga ili kukabiliana na sheria hii ya aibu. Kupitia kuelimisha na kufichua matokeo yake, aliwafunulia wananchi uhalisia wa utawala wa Pahlavi uliokuwa tegemezi kwa wageni na uliopinga maslahi ya wananchi.”

Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Markazi, akieleza kuwa kapitulasyon ilimaanisha kuwapa washauri wa Marekani nchini Iran kinga dhidi ya kufunguliwa mashtaka na kuchukuliwa hatua za kisheria, aliongeza: “Sheria hii ilihoji uhuru na heshima ya kitaifa ya nchi, na kuunda mazingira ambayo raia wa Marekani waliondolewa katika wajibu wa kutii sheria na kufurahia haki sawa na wananchi wa Iran.”

Ayatullah Dori Najafabadi, akizungumzia hotuba ya kihistoria ya Imam Khomeini (r.a.) ya kupinga sheria hiyo, alibainisha: “Imam Khomeini alitangaza waziwazi kwamba kupitishwa sheria ya aina hii ilikuwa sawa na kuiuza Iran pamoja na wananchi wake. Kupitia msimamo huo wa kishujaa, alifichua sura halisi ya Marekani ya kiburi cha kutawala na kutaka kuwatawala wengine.”

Akizungumzia tarehe 13 Aban na nafasi yake katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: “Siku hii ni ukumbusho wa mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu wa kimataifa, pamoja na msisitizo juu ya uhuru, heshima na mamlaka ya kitaifa. Ni lazima vipengele vya kihistoria na kisiasa vya tukio hili vifafanuliwe kwa kizazi cha vijana.”

Shahada ya Ayatullah Haj Agha Mustafa Khomeini: Hatua muhimu katika mchakato wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Dori Najafabadi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia kumbukumbu ya mwaka wa kuuawa kishahidi Ayatullah Haj Agha Mustafa Khomeini, mwana wa Imam Khomeini (r.a.), alisema: “Kuuawa kwake kishahidi katika mji mtakatifu wa Najaf kulizua wimbi la maandamano na hasira kubwa miongoni mwa wananchi wa Iran. Vikao vya kumuenzi shahidi huyo viligeuka kuwa fursa ya kupanua mapambano ya kimapinduzi na kuimarisha harakati ya Kiislamu.”

Akieleza kwamba Ayatullah Haj Agha Mustafa Khomeini alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri wa kielimu katika Hawza, aliongeza: “Alikuwa na kipawa, ujuzi na uwezo mkubwa katika elimu za Kiislamu. Alikuwa na tafiti na shughuli zenye thamani katika nyanja za fiqhi, elimu ya misingi ya fiqhi (Usul al-Fiqh), tafsiri ya Qur’ani, falsafa na irfani.”

Mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Markazi, akizungumzia nafasi yake ya kielimu na kiroho, alisisitiza: “Ayatullah Haj Agha Mustafa Khomeini alikuwa hazina yenye thamani kubwa kwa Uislamu, Hawza na harakati ya Imam Khomeini (r.a.). Kumbukumbu yake na njia aliyopitia vinapaswa kuendelea kuhifadhiwa na kuenziwa daima.”

Mafunzo kutoka katika Khutba ya Bibi Fatimah Zahra (s.a.) kuhusu Uimamu, Wilaya na Kuwajibika

Ayatullah Dori Najafabadi, katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, akizungumzia khutba ya Bibi Fatimah Zahra (s.a.), alisisitiza umuhimu wa mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.) katika kutambua haki na batili, pamoja na kubainisha vigezo sahihi vya maisha ya mtu binafsi na ya kijamii.

Akizungumzia nafasi ya khutba hiyo katika kufafanua mafundisho ya dini na masuala yanayohusiana na Uimamu na Wilaya, alisema: “Maneno ya Bibi Zahra (s.a.) yamejaa mafundisho ya kina ya dini na yanaonesha namna alivyokuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa jamii ya Kiislamu. Maneno yake yanampa mwanadamu vigezo kama vile uaminifu, ukweli na kutimiza ahadi, vinavyomwezesha kutambua njia ya haki.”

Akizungumzia maudhui ya maneno yaliyotolewa katika khutba ya Hadhrat Zahra (s.a.) kuhusu matokeo ya kujitenga na kutoshirikiana kwa wananchi katika kufuata njia ya Wilaya, aliongeza: “Kama vikwazo vilivyokuwa mbele ya Amirul-Muuminin Ali (a.s.) vingeondolewa na jamii ya Kiislamu ingenufaika na uwezo na vipawa vyake, basi uwezekano wa kuisimamia jamii kwa misingi ya uadilifu na mafundisho halisi ya Kiislamu ungekuwa mkubwa zaidi.”

Ayatullah Dori Najafabadi, mwishoni mwa hotuba yake, alisisitiza kuwa kupitia upya historia ya mwanzo wa Uislamu na kunufaika na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.) ni jambo la lazima katika kutambua wajibu wa kijamii na kisiasa katika jamii ya Kiislamu. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kushikamana na vigezo vya haki, uadilifu, kustahili na kuwajibika katika nyanja zote.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha